Saturday, September 28, 2013

YANGA KUWAVAA RUVU SHOOTING LEO

Young Africans leo itashuka dimbani kucheza na timu ya Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya muendelezo ya michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania 2013/2014.
Mabingwa watetezi Yanga ina pointi 6 baada ya kucheza michezo mitano kushinda mmoja, kutoka sare michezo mitatu na kupoteza mchezo mmoja itakutana na Ruvu Shooting ambayo imejikusanyia pointi 9 baada ya kushinda michezo mitatu na kupoteza michezo miwili.
Young Africans ambayo leo itashuka dimbani kuhakikisha inasaka pointi 3 muhimu ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kutetea ubingwa wake, jana iliendelea na mazoezi katika viwanja vya shule ya Sekondari Loyola -Mabibo jijini Dar es salaam.
Wachezaji wote waliingia kambini katika hosteli zilizopo makao makuu ya klabu kujiandaa na mchezo huo wa leo ambao ni muhimu kwa watoto wa Jangwani kuhakikisha wanapata ushindi.
Kocha wa Yanga mholanzi Ernie Brandts amesema kikosi chake kimekamilika katika kila idara kuelekea kwenye mchezo wa leo na kusema ameyafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita.
Wapenzi, wanachama na washabiki wa Young Africans mnaombwa kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kuja kuwashangilia vijana watakapokua wanapambana na timu ya maafande wa Ruvu Shooting.

No comments:

Post a Comment