Young Africans ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu
huu wa 2012/2013 leo imetoka sare ya 0-0 dihi ya timu ya Polisi Morogoro
katika mchezo uliofanyika leo jioni katika uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na
washabiki wengi wa soka kutoka mkoa wa Dar es salaam na mikoa ya jirani,
umeishia kwa sare hiyo ya pasipo kufungana huku mwamuzi wa mchezo huo
Dominic Nyamisana na wasaidizi wake wakishindwa kulimudu pambano hilo
kutokana na kutokua makini.
Watoto
wa jangwani waliuanza mchezo kwa kasi kwa lengo la kupata bao la mapema
na katika dakika ya tatu mchezo, Hamis Kiiza alishindwa kuipatia Yanga
bao la kuongoza kutokana na kutokua makini katika umaliziaji.
Polisi
nayo ilijaribu kufanya mashambulizi ya kushtukiza lakini umakini wa
walinzi wa Yanga ulikuwa kikwazo kwao kuweza kumfikia mlinda mlango Ally
Mustafa 'Barthez'
Yanga
iliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa timu ya Polisi lakini
kutokua makini kwa washambuliaji wa Yanga Saimon Msuva, Said Bahanuzi,
Hamis Kiiza na Nizar Khalfani ulishindwa kuipatia Yanga bao .
Mpaka mpira unakwenda mapumziko, wenyeji Polisi Morogoro 0 - 0 Young Africans.
Kipindi
cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko kwa kumuingiza Stephano
Mwasika aliyechukua nafasi ya Nizar Khalfani, mabadiliko hayo
yaliongeza uhai kwa timu ya Yanga ambapo iliweza kufanya mashambulizi
mengi langoni mwa timu ya Polisi.
Baada ya Yanga kuwa inafanya
mashambulizi mengi langoni mwa timu ya Polisi na kusababisha kupata kona
nyingi mfululizo, wachezaji wa Polisi waliamua kuwa wanajiangusha kila
dakika ili kupoza kasi ya mchezo huku mwamuzi akionekana kutokujali kwa
tabia hiyo ya wachezaji.
Polisi waliendelea kucheza kwa kupoteza
muda hali iliyopelekea kupoteza radha ya mchezo, dakika za majeruhi
Yanga ilifanya mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa Polisi lakini
mashambulizi hayo hayakuweza kuipatia bao.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Polisi Morogoro 0 - 0 Young Africans.
Kwa
matokeo hayo ya leo Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi
Kuu ya Vodacom baada ya kufikisha pointi 49 ikiwa ni pointi 6 mbele ya
timu ya Azam inayokamata nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 43.
Kikosi cha Young Africans:
1.Ally Mustafa 'Barthez', 2.Mbuyu Twite, 3.David Luhende, 4.Nadir
Haroub 'Cannavaro', 5.Kelvin Yondani, 6.Athumani Idd 'Chuji', 7.Saimon
Msuva, 8.Frandk Domayo, 9.Said Bahanuzi/Didier Kavumbagu, 10.Hamis
Kiiza, 11.Nizar Khalfani/Stephano Mwasika
No comments:
Post a Comment